Tuesday, January 03, 2006

HAZINA PEVU

Hazina pevu, haiji kwa haraka haraka.Ni sehemu ya uvumilivu unaojikita katika kutafuta uimara na mhimili mkuu wa uang'avu wa akili.Ni sawa na embe dodo lililoiva. ukilila lingali bichi ni kama unameza klorokwini. Ukipata bahati ya kulilinua lilioiva mtini au ukalichuma mwenyewe mtini utadhani unameza vidonge vya magnezium, vinakupa unafuu nafsini na tumboni.

Hazina ya Tanzania si madini yanayochumwa na kutafutwa kwa udi na uvumba na wananchi pamoja na wawekezaji nchini, si mito, maziwa,mbuga au milima tuliokuwa tunaimba huko secondary na msingi kujivunia utajiri wetu, si mabonde na misitu lukuki iliojaa nyuki na wadudu wa kila aina, si chochote mungu alichotupa kionekanacho machoni na kisichooenekana katika uso wa ardhi bali ni hazina ya akili na fikra pevu za watu wa Tanzania.

Tunaweza kuwa na yote hayo na kwa sasa mwenyezi Mungu hakutunyima. Lakini kama hatuna maarifa, ujuzi, adabu ya akili na utulivu wa mipango tutabaki tukiwa na utajiri kwenye ramani ya nchi na vichwani mwetu isioonekana hadharani, au kuonekana kubadilisha maisha yawatu.

Kama ambavyo inachuka majira embe kuiva na kuonekana kufaa kuliwa ndivyo inavyochukua muda, nguvu, mali na ari na mali kuja kuwa na akili pevu kulisaidia taifa,.Kwa bahati mbaya Tanzania leo bado watu wanafikiri serikali yao tukufu inaweza kufanya au kuwafanyia maendeleo yao, la hasha, wananchi ndo wawe mbele kujipangia maendeleo yao ili kwa ujumla wake serikali iwasaidie kuweka mazingira huru na sawa katika kutumia utajiri wetu wa asili.

Kama serikali inakuwa na mipango ya maendeleo kwa muda kadhaa, kama ambavyo tuna dira ya 2025 ya kupunguza umaskini ndivyo hivyo kila mwananchi ajipangie dira yake atakavyotekeleza mipango yake ya muda mrefu na mfupi na aiambie serikali jinsi alivyoshindwa na kwa nini na ni wapi anahitaji msaada na siyo kulalamika tu bila kuchukua hatua yoyote ya kimaendeleo.

Twahitaji kurudi shule kupata upevu wa akili, shule yenyewe ni kutafuta maarifa popote ulipo, iwe kijijini au mjini, shuleni au nyumbani.

Hima watanzania na dunia , Dunia haitabadilika na kustaarabika zaidi na kuwa paradiso ndogo kama akili pevu na hazina mwanana ya nuru ya elimu, ujuzi, maarifa na ufundi havitatawala nyoyo za wakazi wa duniani.

Ni akili pevu tu na hazina zake ndizo zitakazoipa dunia na watu wake mwangaza na matumaini ya kuishi katika dunia ya ubabe wa fedha, silaha,na siasa za hali ya juu.

Akili pevu si wingi wa digrii na diploma , ni hali ya utambuzi wa mahitaji halisi ya dunia na watu wake na mchango chanya kwa kila tendo ulitendalo kwa dunia na watu wake kwa dhamana ndogo uliopewa na Mungu, watu, kikundi au familia.

Nashawishika kutamka kuwa wala rushwa, wezi, majambazi , wabaguzi wa rangi za ngozi ya miili yetu na ubaguzi mwingine wowote, wazembe kwa majukumu waliopewa,wasaliti, wote wanaangukia kwenye ukosefu wa akili pevu bila kujali idadi ya madarasa aliokaa shuleni.

1 Comments:

Blogger mwandani said...

Umeongea. Kwanza watu,kwanza akili, mengine yanafuata hapo

11:28 PM  

Post a Comment

<< Home